Tuesday 10 December 2013

CHIMBUKO LA RIWAYA YA KISWAHILI

CHIMBUKO LA RIWAYA YA KISWAHILI.
Katika mjadala huu, tutajikita zaidi kwa kutoa maana ya riwaya kutoka kwa wataalamu mbalimbali, maana ya riwaya ya Kiswahili, maana ya chimbuko, Kisha mjadala huu utaelekea zaidi katika kuelezea chimbuko la riwaya ya Kiswahili kutokana na wataalamu mbalimbali waliopata kueleza asili ya riwaya hiyo ya Kiswahili, na hicho ndio kitakachokuwa kiini cha mjadala wetu. Mwisho kabisa hitimisho la mjadala. 
Kwa kuanza na maana ya riwaya imejadiliwa kama ifuatavyo:
Wamitila (2003:178), anasema riwaya ni kazi ya kinathari au kibunilizi ambayo huwa na urefu wa kutosha, msuko uliojengeka vizuri, wahusika wengi walioendelezwa kwa kina, yenye kuchukua muda mwingi katika maandalizi na kuhusisha mandhari maalumu.
Muhando na Balisidya (1976:62), wanasema riwaya ni kazi ya kubuni, ni hadithi ambayo hutungwa kufuatana na uwezo wa fanani kuibusha mambo kutokana na mazoea au mazingira yake. Wanaendelea kusema kuwa riwaya yaweza kuanzia maneno 35,000 hivi na kuendelea.
Nkwera (1978:109), anasema riwaya ni hadithi iliyo ndefu kuweza kutosha kufanya kitabu kimoja au zaidi. Ni hadithi ya kubuniwa iliyojengwa juu ya tukio la kihistoria na kuandikwa kwa mtindo wa ushairi iendayo mfululizo kwa kinaganaga katika kuelezea maisha ya mtu au watu na hata taifa. Anaendelea kusema kuwa riwaya ina mhusika mkuu mmoja au hata wawili.
Senkoro, anasema riwaya ni kisa ambacho urefu wake unakiruhusu kitambe na kutambaa vizingiti vingi vya maisha kama apendavyo mwandishi wake. Anaendelea kusema kuwa ni hadithi ndefu ya kubuni, yenye visa vingi, wahusika zaidi ya mmoja na yenye mazungumzo na maelezo yanayozingatiwa kwa undani na upana wa maisha ya jamii.
Hivyo inaonyesha kuwa ili kujua maana ya riwaya ni vyema kuzingatia mambo kadhaa ambayo ndiyo ya msingi, na mambo hayo ni; lazima riwaya iwe na lugha ya kinathari, isawiri maisha ya jamii, iwe na masimulizi ya kubuni na visa virefu, wahusika zaidi ya mmoja, iwe na mpangilio na msuko wa matukio, lazima na maneno kuanzia elfu thelathini na tano na kuendelea, na mwisho riwaya ni lazima ifungamane na wakati yaani visa na matukio ni lazima viendane na matukio.
Baada ya kuangalia maana ya riwaya kutokana na wataalamu mbalimbali sasa ni vyema kutoa maana ya riwaya ya Kiswahili kabla ya kujadili chimbuko la riwaya.
Riwaya ya Kiswahili ni ile ambayo inafungamana na utamaduni wa jamii ya waswahili katika lugha ya kiswahili ambao hupatikanakatika nchi ya Afrika mashariki. Pia ni ile riwaya ambayo inawahusu waswahili wenyewe.
TUKI (2004:48) inasema chimbuko la maana yake ni mwanzo au asili.
Tanzu za asili zinaonyesha kuwa ndio zilichangia kwa kiasi kikubwa sana katika kuibua riwaya za Kiswahili. Na yafuatayo ni mawazo ya wataalamu mbalimbali juu ya chimbuko la riwaya ya Kiswahili.
Madumulla (2009), ameeleza kuwa riwaya ilitokana na nathari bunifu simulizi kama vile hadithi, hekaya, na ngano inayosimuliwa kwa mdomo. Anaendelea kusema kuwa fasihi ilitokana na maandiko ya fani ya ushairi hususan ni tendi za Kiswahili katika hati za kiarabu kwa sababu ndiyo maanadishi yaliyotamba katika pwani ya afrika mashariki. Wazungu na waarabu hawakubadilishana maarifa kwa urahisi na hivyo pakapelekea kuwa na majilio ya taratibu za maandiko ya kinathari. Mwanzoni riwaya zilitafsiriwa kwa Kiswahili toka katika lugha za ulaya na kufanya riwaya za Kiswahili kutokea.Mfano wa riwaya hizo ni kama vile; Habari za mlima iliyoandikwa na Sheikh Ali Bin Hemed (1980).
Senkoro (2011) anaeleza kuwa riwaya zilizuka kutokana na maendeleo na mageuzi ya kiutamaduni, uchangamano wa maisha ya kijamii, kisiasa, kiuchumi, na kiutamaduni yaliyopelekea haja ya kimaudhui zaidi ya ngano na hadithi fupi.Anaendelea kusema kuwa riwaya za kwanza zilitafsiriwa toka riwaya za kizungu mpaka za kiswahili. Anasema riwaya mojawapo ni ile ya James Mbotela ya Uhuru wa Watumwa. Ndiyo riwaya ya kwanza kutafsiriwa kwa Kiswahili.Pia  anaeleza kuwa  riwaya ni utanzu uliozuka kutokana na hali mahususi za kijamii.Riwaya kama ile ya kiingereza ya Robinson Crusoe iliyoandikwa na Daniel Defoe ni miongoni mwa riwaya za mwanzo. Anasema riwaya ilizuka kutokana na maendeleo na mageuzi ya kiutamaduni na viwanda.Suala la ukoloni na uvumbuzi pia liliumba hali ambazo zilihitaji kuelezwa kwa mawanda mapana zaidi ya yale ya ngano na hadithi fupi. Kupanuka kwa usomaji hasa wakati wa vipindi vya mapinduzi ya viwanda huko ulaya kilifanya waandishi waandike maandiko marefu kwani wakati huo ndipo walipoibuka wasomaji hasa wanawake waliobaki majumbani wakati waume zao walipokwenda viwandani kufanya kazi.
Mulokozi (1996) anaeleza kuwa chimbuko la riwaya ya Kiswahili lipo katika mambo makuu mawili ambayo; ni fani za kijadi za fasihi pamoja na mazingira ya kijamii.
Fani za kijadi za fasihi, Mulokozi anaeleza kuwa riwaya haikuzuka hivihivi tu bali ilitokana na fani za masimulizi yaani hadithi, na ndipo zikapatwa kuigwa na watunzi wa riwaya wa mwanzo.Fani hizo zilizopata kuchipuza riwaya za mwanzo ni kama vile; riwaya za kingano, tendi, hekaya, visakale, historia, sira, masimulizi ya wasafiri, insha na tafsiri.
Ngano, Mulokozi anasema, kuwa ni hadithi fupi simulizi pia huwa ni hadithi za kubuni na nyinga hasa zinawahusu wanyama wakali, pia zinahusu malaika, binadamu, mazimwi na majini. Anasema kuwa mara nyingi ngano huwa na msuko sahihi na wahisika wake ni bapa na wahisika hao ni mchanganyiko wa wanyama, mazimwi na binadamu. Anatolea mfano wa ngano zilizo chukua visa vya kingano kuwa ni kama vile riwaya ya Adili na Nduguze ya Shaban Robart (1952), Lila na Fila ya Kiimbila (1966), Kusadikika ya Sharban Robart (1951) na baadaye yakafuata machapisho mengine kama vile; Mfalme wa Nyoka ya  R.K. Watts. Dhamira za riwaya za kingano ni kama vile choyo, mgongano wa kimawazo na tama.
Hekaya, ni hadithi za kusisimua kuhusu masaibu na matukio ya ajabu yaani yasiyokuwa ya kawaida. Mara nyingi masaibu hayo hufungamanishwa na mapenzi. Pia hekaya ni ndefu kiasi yaani sio ndefu kiasi cha kama riwaya. Katika jamii ya waswahili hekaya zilikuwa zimeenea sana kipindi cha kabla ya ukoloni. Mifano ya hekaya ni kama vile; Hekaya za Abunuasi ya C.M.C.A. 1915, Sultan Darai (1884), Kibaraka ya (1896) na hekaya ya Jonson, F. na Brenn, E.W. katika hekaya ya Alfa-Lela-Ulela ya kuanzia 1929. Hizo ndizo baadhi ya hekaya za mwanzo lakini baadaye ziliathili riwaya za Kiswahili kama vile; Hekaya ya Adili na Nduguze ya Sharban Robart (1952), hekaya ya Ueberu Utashindwa ya Kiimbila (1971), na Hekaya ya A.J.Amiri, ya Nahodha Fikirini, (1972).
Tendi (utndi), ni hadithi ya kishairi kuhusu mashujaa wa kihistoria na wa kubuni, ambao waweza kuwa ni wa kijamii au kitaifa. Kwa kawaida baadhi ya tendi zina sifa za kiriwaya ila tu badala ya kuwa na umbo la kinathari zenyewe zina umbo la kishairi. kuna tendi za aina mbili ambazo ni tendi andishi na tendi simulizi. Riwaya pevu kama tendi husawiri mawanda mapana ya kijamii na kihistoria.Huwa na wahusika wababe yaani mashujaa wenye kuwakilisha pande zinazopingana.Mfano wa tendi ni kama vile; Utendi wa Vita vya Wadachi Kutamalaki Mlima ya Hemedi Abdallah, (1895), Utendi wa rasil ‘Ghuli, utenzi wa Fumo liyongo wa Mohamed Kijumwa K. (1913).Tendi katika riwaya za Kiswahili imetumia wahusika wawili tu ambao ni wahusika wa kubuni na wale wa kijadi wa kiafrika.
Visasili, hizi ni hadithi zinazohusu asili na hatima ya watu, vitu, viumbe, ulimwengu na mataifa, na pia huangalia uhusiano wa wanadamu na mizimwi pamoja na miungu. Hadithi za kivisasili zinapoonyeswa huaminika kuwa yakweli tupu hasa kwa kusimulia matukio mengi ya kiulumwengu.
Mfano wa visasili; Lila na Fila ya Kiimbila (1966) ambayo imekopa motifu ya asili ya ziwa ikimba huko Bukoba.Hadithi ya Mungu wa Kikuyu huko Kenya. Rosa Mistika ya Kezilahabi (1971), Nagona (1987) na Mzingile (1991), Siku ya Watenzi Wote ya Sharban Robart.
Visakale, ni hadithi ya kale kuhusu mashujaa wa taifa, kabila au dini.Mara nyingi visa kale huchanganya historia na masimulizi ya kubuni, na hadithi hizi hupatikana karibu katika kila kabila kila lugha.Baadhi ya visakale vya Kiswahili masimulizi huhusu chimbuko la miji ya pwani, mijikenda, mwinyi mkuu huko Zanzibar.Visa kama hivi ndivyo vinavyopelekea kuandikwa kwa riwaya za kiswahili. Mfano wake ni riwaya ya Abdalla Bin Hemed bin Ali Ajjemy (1972) katika kitabu cha Habari za Wakilindi, Kisima cha na Giningi ya M.S.Abdulla (1968) na ile Hadithi ya Myombekela na Bibi Bugonoka na Ntulanalwo na Buhliwali (1980) ya A. Kitereza.
Visasuli, hizi ni hadithi zozote ambazo huelezea chimbuko au asili ya kitu chochote, na maranyingi visasuli havina uzito wowote kulinganisha na visasili.mfano wake ni; kwanini paka anapenda kukaa jikoni (mekoni), Kwa nini mbuni hana mabawa yaani hapai angani, kwa nini kima anamuogopa mamba, kwanini mbwa kuishi na binadamu, kwa nini fisi hupenda kula mifupa. Katika hadithi hizi watu huwa hawaamini sana bali wanachukulia kuwa ni utani tu.
Masimulizi ya kihistoria, haya ni masimulizi ya matendo ya, mwanadamu katika muktadha wa wakati, na ni fani muhimu sana katika jamii yeyote ile.Masimulizi halisi ya kihistoria yaweza kuwa ni ya mdomo au hata maandishi na yote huwa ni chemichemi nzuri ya riwaya. Mfano wa riwya hizo ni; Habari za pate za Fumo Omari Nabhany (1913) ambayo yalikuwa ni maandishi ya masimulizi na uchambuzi.Riwaya zingine zilizoathiriwa na matukio ya kihistoria ni; Uhuru wa Watumwa ya J. Mbotela (1934), Kifo cha Ugenini ya O. Msewa (1977), Kwa Heri Iselamagazi ya B. Mapalala (1992) na Miradi Bubu ya Wazalendo ya G. Ruhumbika (1992).
Sira, ni masimulizi ya kweli kuhusu maisha ya mtu au watu. Sira huweza kuwa wasifu yaani zinazohusu habari za maisha ya mtu zikisimuliwa na mtu mwingine au zaweza kuwa tawasifu yaani habari za maisha ya mtu zikisimuliwa nayeye mwenyewe. Sira iliathiri kuchipuka kwa riwaya hasa kwa kuonyesha masilimulizi ya maisha ya mtu toka utotoni mpaka uzeeni. Masimuliza ya riwaya hizi yalikuwa katika masimulizi na hata katika maandishi pia kwa maana kabla ya ukoloni yalikuwepo maandishi yaliyohusu maisha ya mitume na masahaba. Mifano ya hadithi hizi ni; Kurwa na Doto ya M.S.Farsy (1960), Rosa Mistika ya Kezilahabi (1971),Kichwa Maji ya Kezilahabi (1974) pamoja na Dunia Uwanja wa Fujo (1975),Mzimu wa Baba wa Kale ya Nkwera (1967),na riwaya ya Maisha Yangu baada ya Miaka Hamsini ya Sharban Robart (1951).
Msimulizi ya wasafiri, hizi ni habari zinazosimulia masibu nya wasafiri katika nchi mbalimbali. Hekaya za riwaya chuku za kale zilisaidia kukuza riwaya. Mfano Alfa –Lela –Ulela na hadithi ya Robinson Kruso huko 1719 ilihusu safari ya baharini ya mhusika mkuu ambaye baadaye merikebu aliyokuwemo ilizama, ndipo akalazimika kuishi peke yake katika kisiwa kidogo. Na katika riwaya za Kiswahili kuna baadhi ya riwaya za masimulizi kama vile; Mwaka katika Minyororo ya Samweli Sehoza (1921), Tulivyoona na Tulivyofanya Uingereza (1932) ya Martin Kayamba. Na uhure wa Watumwa na Kwa Heri Eselamagazi.
Insha, ni maandiko ya kinathari yenye kuelezea, kuchambua au kuarifu kuhusu mada Fulani. Zipo insha nyingi kama vile, makala, hotuba, tasnifu, michapo, barua, sira maelezo n.k insha nyingi ni fupi mfano kuanzia maneno kama 500 na 10000 japo zingine zaweza kuwa ni ndefu kiasi cha kuwa tasnifu za kufikia kiwango cha kuwa kitabu. Mfano wa insha ni Siku ya Watenzi Wote ya Sharban Robert na Kichwa Mji ya Kezilahabi.
Shajara, ni kitabu cha kumbukumbu za matukio ya kila siku .Uandishi wa shajara ulianzia huko Asia na baadaye ndio ulipopata kuibuka ulimwenguni kote. Jadi hii ya kiasia iliathiri utunzi wa riwaya hasa zile za kisira. Mfano wa shajara ni ile iliyotungwa na Lu Shun iitwayo Shajara ya Mwendawazimu (1918).
Romansia (chuku) hii ni hadithi ya mapenzi na masaibu ya ajabu.Zikua maarufu sana huko Uingereza hasa karne ya 6 na 12 na Ufaransa pia zilikuwepo na pamoja na China ambapo hadithi zilizofanana na riwaya zilitungwa.mfano hadithi za Hsiao-shuo.Watunzi wa riwaya za kisasa zimekuwa na mafanikio makubwa sana kutokana na riwaya hizo za chuku hii ni kwa sababu watunzi wengi wlikuwa wamesoma kazi nyingi za riwaya za wakati ule.
Drama, maigizo mengi hasa ya tamthiliya yaliathiri sana riwaya hasa kwa upande wa usukaji wa matukio na uchanganyaji wa ubunifu na uhalisia. Mfano ni riwaya nyingi za Charles Dickens zina msuko uliosanifiwa kwa uangalifu kama msuko wa tamthiliya.
Baada ya kujadili fani za kijamii hatuna budi sasa ya kujadili mazingira ya kijamii kama yalivyopatwa kuelezwa na Mulokozi.Anaeleza kuwa, kufikia karne ya 16 fani za kijamii zilikuwa zimekwisha enea na kufahamika katika maeneo mengi, hivyo kulihitajika kuwe na msukumo wa kijamii, kiteknolojia na kiuchuni. Msukumo huo wa kundeleza fani za kijadi ulikuwa ni wa aina tatu ambao ni;
Ukuaji mkubwa wa shughuri za kiuchumi huko ulaya, ukuaji huo ulifungamana na biashara ya baharini ya mashariki ya mbali na kuvumbuliwa kwa mabara mawili ya amerika na ukuaji wa viwanda hasa vya nguo huko ulaya. Mabadiliko haya yalizua tabaka jipya la mabwanyenye waliomiliki viwanda na nyenzo nyingine za kichumi.Tabaka hilo lilihitaji fani mpya za fasihi, lilikuwa na wakati wa ziada wa kujisomea, uwezo wa kifedha wa kujinunulia vitabu na magazeti.Hivyo tangu mwanzo ilitawaliwa na ubinafsi uliojidhihirisha kiitikadi. Kwa mfano Robinson Kruso ni riwaya ilyosawili ulimbikizaji wa mwanzo wa kibepari. Ilimhusidhs muhusika asiye staarabika aitwaye Fraiday au Juma. Ubinafsi huu ulijitokeza pia katika utungaji wake, na haikusomwa hadharani bali kila mtu alijisomea mwenyewe chumbani mwake.
Mageuzi ya kijamii na kisiasa, mabadiliko haya yalifungamana na mabadiliko ya kiuchumi. Mataifa ya ulaya yalianza kujipambanua kiutamaduni na kisiasa yaliyojitenga na dola takatifu ya kirumi.Mabadiliko hayo yalianza kujenga utamaduni wa kitaifa na mifumo ya elimu iliyo hiyaji maandishi katika lugha zao wenyewe.Mfano wa mageuzi ya kijamii na kisiasa iliyofanyika ni kama vile; Misahafu ya Dini Kama Biblia ilanza kutafsiriwa kwa lugha za ulaya, Martin Lther alichapisha Biblia kwa lugha za kidachi miaka ya 1534. Hivyo basi inaonyesha kuwa kadiri elimu ilivyopanuka na nduvyo wasomaji wa vitabu walivyoongezeka na kufanya kuwe hadhira kubwa nzuri ya wasomaji na watunzi wa riwaya.
Ugunduzi wa teknolojia ya upigaji chapa vitabu, yaani kwa kutumia herufi iliyoshikamanishika.Ugunduzi huu uliofanywa na Johnnes Gutenberg huko ujerumani mwaka 1450 uliorahisisha kazi ya uchapaji vitabu katika nakala nyingi nakuondoa kabisa haja ya kunakili miswada kwa mikono. Bila ugunduzi huo kufanyika haingewezekana kuchapisha riwaya nyingi na kuzieneza kwa bei nafuu. Mifano ya riwaya hizo ni kama vile; Pamela ya Samwel Richardson (1740).
Kutokana na wataalamu mbalimbali kuelezea chimbuko la riwaya ya Kiswahili, inaonekana kuwa, riwaya ni utanzu wa fasihi ambao kuzuka kwake kulifungamana na fani za kijadi pamoja na mazingira ya kijamii. Fani za kijamii kama vile, ngano, visasili, visasuli, visakale, insha, na nyinginezo zizosimuliwa bila ya kuandikwa kabla ya karne ya 16, zilichochewa na kupewa mwendelezo baada ya kukua kwa sayansi na teknolojia huko ulaya, hasa baada ya ugunduzi wa mitambo ya kupiga chapa kazi za fasihi.   
MAREJEO
Madumulla, J.S. (2009), Riwaya ya Kiswahili, Historian a Misingi ya Uchambuzi. Nairobi: Sitima Printer and stations L.td.
Mulokozi, M.M. (1996), Utangulizi wa Fasihi ya Kiswahili. Dar es Salaam. TUKI.
Mhando, P. na Balisidya, (1976), Fasihi na Sanaa za Maonyesho. Dar es Salaam: Tanzania Publishing House.
Nkwera, F.V. (1978), Sarufi na Fasihi Sekondari na Vyuo. Dar es Salaam: Tanzani Publishing House.
TUKI, (2004), Kamusi ya Kiswahili Sanifu. Nairobi.Kenya:Oxford University Press.
Senkoro, F.E.M.K. (2011), Fasihi Andishi.Dar es Salaam.Kauttu L.t.d.
Wamitila, K.W. (2003), Kamusi ya Fasihi, Istilahi na Nadharia. Nairobi: Focus Publication.  

3 comments: